Zachembe: Faiza Ally Ex Sugu Ala za Uso Baada ya Kuvaa Pempasi
ULIMWENGU wa kisasa haukuweza kuiweka kando Tanzania, hasa baada ya teknolojia kufika na kutumiwa ipasavyo na jamii yetu. Hii imefanya kuzaliwa kwa ule msemo kuwa dunia imekuwa kijiji, kwa maana kwamba sasa unaweza kujua au kuona kila kitu kilichopo duniani kupitia simu yako iliyo kiganjani.
Simu hizi, hasa kwa vijana, zimewasogeza karibu zaidi na wenzao duniani kote, kiasi kwamba siyo jambo la ajabu mtu akiwa Kariakoo, anajipiga picha na baadaye anamtumia mwenzake aliyeko kule Singida.
Vijana wako bize na Twitter, Facebook, Instagram, WhatApp na nini sijui, ili mradi kila mmoja ni mtu wa kisasa. Mabadiliko haya ya teknolojia, yametubadilishia hadi staili ya maisha, kiasi kwamba unashangaa mitindo inayofanywa kwa malengo maalum kule Ulaya, kwetu tunaichukulia kama fasheni, tunaiga tu ili mradi tuonekane tunaenda na wakati.
Ulaya na Marekani wanamwagiana maji ya baridi katika msimu maalum kwa ajili ya harambee mbalimbali za kusaidia jamii. Kwa wenzangu na mimi wasiojua, muda mwingi wa mwaka Ulaya ni baridi, tena baridi kwelikweli, kwao kumwagiwa maji baridi ni zaidi ya adhabu, lakini katika kuonyesha mtu yuko tayari kuchangia kampeni mbalimbali za kusaidia jamii, hukubali kumwagiwa maji hayo.
Unashangaa mara moja Bongo nako, ambako ni joto la kufa mtu, eti na wenyewe wanaiga kumwagiana maji baridi, wakati kimsingi ni afueni kwa mmwagiwaji, vinginevyo wangemwagiwa maji ya moto!
Tabia hii ya kuiga bila kuchuja imekuja kwa wasanii wetu, hasa hawa wa muziki wa kizazi kipya na waigizaji wa filamu.
Sijui imetokea wapi, lakini limekuwa tendo jipya hivi sasa kuona katika sherehe zao mbalimbali, wanammwagia bia anayesherehekea, katika kuonyesha wenzake wanamuunga mkono.
Sijui hii staili, lakini sidhani kama ni sawa mtu uwe umeupara kwa ajili ya sherehe, halafu eti tena umwagiwe pombe mwili mzima. Hili limetokea juzijuzi kwa Baby Madaha na wengine wengi huko nyuma. Kwa maoni yangu, huu ni ukisasa wenye ulimbukeni wa kutosha ndani yake.
Lakini funga kazi zaidi imejitokeza juzikati, baada ya msanii mmoja asiye na jina kubwa, anayefahamika kwa jina la Faiza Ally kuingia ukumbini akiwa amevalia kama watoto wachanga wanavyovalishwa, yaani wenyewe akina mama wanasema Pempasi.
Dah, Faiza aliingia katika ukumbi aliouandaa na kujitokeza mbele ya watu aliowaalika akiwa katika namna ambayo mtu muungwana asingetegemea. Alipoulizwa kisa cha kufanya hivyo, akadai eti kwa kuwa ni siku yake ya kuzaliwa, ameona ni vyema kama atavaa mavazi hayo maalum kwa watoto wachanga!
Labda kwa vile sherehe kama hizi huwakutanisha mhusika na marafiki zake, lakini unapodiriki kuruhusu picha na kuridhia kutumika hadharani, ni lazima kuwepo na kitu kingine cha kujiuliza, hasa unapomzungumzia msanii wa Kitanzania.
Watu wanaiga uzungu, kwa sababu ni wazungu peke yao ambao tunajua ni wendawazimu kiasi kwamba wanaweza kutembea uchi barabarani halafu wenyewe wakaona poa tu. Kwa Mtanzania, ni aibu na fedheha kuvaa mavazi ambayo unajua wazi kuwa hata wazazi wako hawawezi kukuunga mkono.
Tunaiga ujinga, tunaacha weledi. Tunawaiga matendo yao yasiyoendana na utamaduni wetu, lakini hatutaki kuiga jinsi wanavyofanya kazi zao kwa ubora.
Kwa mara nyingine, nitumie fursa hii kuwaomba wasanii wetu kujaribu kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha mila, desturi na tamaduni zetu zinalindwa na kudumishwa. Tusisahau kuwa hao tunaowaiga, wenyewe wanafurahi kweli wanapotuona katika mavazi ya Vitenge na Khanga au nguo za kimasai, kuliko tunavyojitesa kuvaa suruali za kubana na vimini.