Nna hizi stori kumi kutoka MAGAZETINI Tz, Mtanzania, Mwananchi, Nipashe, Habari LEO…
Nna hizi stori kumi kutoka MAGAZETINI Tz, Mtanzania, Mwananchi, Nipashe, Habari LEO…
MTANZANIA
Jeshi la Polisi mkoani Mwanza
limewakamata waganga wa kienyeji 55 wakiwa na viungo vya binadamu
vikiwamo meno na nywele vinavyodaiwa kuwa ni vya watu wenye albino.
Vitu vingine walivyokutwa navyo ni ngozi ya simba, nyumbu, mamba, vibuyu, njuga, vioo, shanga na debe tatu za bangi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola, alisema waganga hao walikamatwa katika wilaya za Mkoa wa Mwanza kwenye msako ulioanza juzi.
Alisema katika msako huo wamefanikiwa
kuwakamata waganga hao wanaodaiwa kupiga ramli chonganishi
zinazosababisha kuchochea matukio ya mauaji kwa albino na vikongwe.
“Katika
msako wa Jeshi la Polisi ulioanza juzi tumefanikiwa kuwatia mbaroni
waganga wa jadi 55 ambapo kati yao tumewakuta na nywele, meno za watu
wenye albino waliouawa katika matukio tofauti mkoani hapa,” Mlowala.
Kamanda huyo wa Polisi alisema waganga
hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili ikiwamo
kumiliki nyara za Serikali kinyume cha sheria pamoja na viungo vya
binadamu.
Mbali na tukio hilo, taarifa kutoka
wilayani Misungwi zinaeleza kuwa watu wanne wamefikishwa kortini mjini
hapa kwa tuhuma za kuuza mafuta maalumu ya ngozi yanayotumiwa na watu
wenye albino.
Mafuta hayo yenye thamani ya Sh milioni tano, ambayo yalitolewa na Hospitali ya Bugando kwa watoto wenye albino wilayani humo.
MTANZANIA
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam jana lilimuhoji Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.Willibrod Slaa, kwa zaidi ya saa sita kuhusiana na tuhuma za mauaji dhidi yake.
Hilo limetokea siku moja baada ya mlinzi binafsi wa Dk. Slaa, Khalid Kagenzi, kueleza jinsi alivyoteswa na walinzi wa Chadema na hata kumuhusisha na tishio la mauaji ya kiongozi huyo.
Dk.Slaa alihojiwa katika Kituo Kikuu cha
Polisi Dar es Salaam jana kuanzia saa 4.00 asubuhi hadi saa 10.00 jioni
huku akiwa amefuatana na mawakili watatu wa chama hicho wakiongozwa na
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Prof. Abdalla Safari. Wengine ni Nyaronyo Kicheere na John Mallya.
Alipofika kituoni hapo, Katibu Mkuu huyo
wa Chadema aliingia moja kwa moja katika chumba maalumu na kuhojiwa na
askari wa upelelezi ikiwamo kuchukuliwa maelezo ya kina kuhusu jinsi
anavyolitambua tukio hilo.
Wakati akihojiwa na polisi, Dk. Slaa
alikuwa akiongozwa na wanasheria wa Chadema ambao muda wote walikuwa
wakisikiliza mahojiano hayo kati ya polisi na kiongozi huyo.
Mahojiano yalipokuwa yakiendelea ndani,
nje ya jengo la polisi walionekana viongozi mbalimbali wa Chadema
wakizunguka, huku wengine wakiingia ndani na kutoka.
“Ndani
kuna mahojiano ya kawaida na anaeleza mazingira ya namna alivyotaka
kuuawa… hivyo anaandika maaelezo ya kile anachokijua yeye,” Safari.
Baada ya mahojiano hayo ilipofika saa
9:40 jioni, Dk. Slaa alitoka ndani kiwa na wanasheria John Malya na
Nyaronyo Kicheere na kuzungumza na waandishi wa habari juu ya mahojiano
yake na polisi.
Alisema utaratibu wa kuandika malalamiko
katika sheria ni kawaida kwa kuwa pande zote zinapaswa kutoa taarifa za
nini wanakifahamu kuhusu tukio lolote.
MWANANCHI
Jukwaa la Wakristo Tanzania limewataka
waumini wake kujiandikisha kwa wingi katika Daftari la Kudumu la
Wapigakura, kuisoma Katiba Inayopendekezwa na kujitokeza kuikataa kwa
kupiga kura ya “hapana”.
Taarifa iliyotolewa na Jukwaa hilo jana na kusainiwa na mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk Alex Malasusa, mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na mwenyekiti wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (CPCT), Askofu Daniel Awet,
imetaja sababu mbili za uamuzi wake kuwa ni muswada wa Mahakama ya
Kadhi kukiuka misingi ya Taifa kuwa na Serikali isiyo na dini, na Kura
ya Maoni kusababisha mgawanyiko.
“Hivyo
basi, Jukwaa linawataka waumini wake wote wajitokeze kwa wingi
kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, waisome Katiba
Inayopendekezwa na kushiriki kikamilifu vipindi vya elimu juu ya Katiba
Inayopendekezwa na kisha wajitokeze kwa wingi kupiga kura ya hapana kwa
Katiba Inayopendekezwa kwa sababu zilizotajwa hapo juu,” linasema tamko hilo la kurasa nne.
Taarifa hiyo imekuja siku moja tu baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda
kutangaza kuwa muswada wa uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi uliokuwa
umeondolewa kwenye mkutano uliopita wa Bunge kwa ajili ya mashauriano
zaidi, utawasilishwa katika vikao vya chombo hicho vinavyoanza Jumanne
ijayo baada ya kufikiwa kwa maridhiano baina ya viongozi mbalimbali wa
dini.
Pia tamko hilo limekuja siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kuiagiza Hazina itoe fedha kwa Tume ya Uchaguzi (NEC) kwa kadri inavyohitaji ili kuiwezesha kukamilisha mchakato wa Kura ya Maoni.
Viongozi wa Jukwaa la Wakristo
walikutana Machi 10, mwaka huu kujadili kwa kina kuhusu hali ya usalama
wa nchi ilivyo sasa na mustakabali wake, Katiba inayopendekezwa na
uanzishaji wa Mahakama ya Kadhi.
MWANACHI
Idadi ya watu waliofariki dunia katika ajali ya Basi la Majinjah imeongezeka na kufikia 50.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema maiti zilizotambuliwa na zile zilizobakia, walipohesabu waligundua idadi yao kufikia 50.
“Tumebaini
kuwa maiti katika ajali ile zimefikia 50 baada ya kuhesabu vizuri zile
zilizotambuliwa na ambazo bado hazijatambuliwa hadi sasa,” Masenza.
Awali, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Robert Salim alisema majeruhi waliopokewa hospitali hapo walikuwa tisa na mmoja ndiye amefariki dunia.
Alisema majeruhi huyo ni Osward Mwinuka (58), aliyefariki dunia usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa.
Dk Salim alisema hali za majeruhi wanne
waliolazwa Hospitali ya Rufaa ya Iringa zinaendelea vizuri wakati
wengine wanne hali zao siyo nzuri na wanatarajia kuwapa rufaa kwenda
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Alisema maiti waliofikishwa hospitalini ni 27 na nane walitambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao wengi wao kutoka Mbeya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi
aliwataja waliotambuliwa kuwa ni Mbezi Deogratius, mkazi wa Soweto
Mbeya, Editha Ngunangwa, mkazi wa Soweto, Mohamed Juma, mkazi wa Mbeya,
Ndenya Sixbert, mkazi wa Mbeya, James Kinyamaguho, mkazi wa Morogoro,
Said Halfan na Abuu Mangula.
Waliojeruhiwa ni
Mustafa Ally, Dominic Shauri, Tito Kyando, Martin Haule, Ipyana Mbamba,
Fadhil Kalenga, Mussa Mwasege, Nehemia Mbuji, Josam Abel, Tumpate
Mwakapala, Nico Hamis na Esther William.
Wengine ni Peter Mwakanale, Kelvin Mwakaladi, Raphael Nerbot, Maga Sebastian, Catherine Mwijungu, Lucy Mtanga, Debora Vicent, Ester na mwanaume ambaye jina lake halikuweza kujulikana kutokana na kuwa katika hali mbaya.
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete
amesema Serikali itajenga nyumba 403 ambazo zimebomolewa na mvua kubwa
iliyonyesha wiki iliyopita katika kijiji cha Mwakata wilayani Kahama na
kusababisha watu 649 kukosa mahali pa kuishi.
Kauli hiyo aliitoa jana kwenye kijiji
cha Mwakata baada ya kutembelea eneo lililoathiriwa na mvua hiyo na
kujionea maisha duni wanayoishi watu hao.
Akizungumza na wananchi waliohudhuria
mkutano wake Rais Kikwete alisema Serikali iko pamoja na wananchi hao na
itahakikisha makazi yao yanarejea katika hali yake ya kawaida kwa
kuwajengea nyumba hizo.
Pia, Rais Kikwete aliagiza Jeshi la Kujenga Taifa(JKT)
wajenge nyumba hizo bila kupitia mkandarasi yeyote kama vile ulivyo
ujenzi wa Serikali kwa kuwa ujenzi wa jeshi unaisha kwa muda mfupi na
hakuna uchakachuaji
Aliwataka viongozi mkoani Shinyanga
kuhakikisha ujenzi huo hautangazwi na kuagiza JKT kwenda kwenye eneo
hilo kufanya tathmini ya ujenzi huo ili uanze mara moja.
Rais Kikwete aliwatoa wasiwasi wananchi
wa Mwakata waliokumbwa na tatizo hilo kwamba Serikali itahakikisha wote
wamepata chakula hadi mwisho watakapolima na kupata mavuno na tukio hilo
wasilihusishe na imani za kishirikina.
Alisema mvua hizo ni za kawaida ambazo
hutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi na si ushirikina hivyo aliwataka
wananchi hao waendelee kuwa na hisia hizo lakini wasilichukulie kwa
uzito swala la ushirikina wakatafuta mchawi wa mvua hiyo
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga
alimwambia Rais Kikwete kwamba mvua hiyo licha ya kuua watu 47 pia
imeharibu mazao hekari 2,332 pamoja na visima 53 vya maji ya kunywa.
Rufunga alisema mpaka kufikia sasa
wahisani mbalimbali wamechangia kwenye tukio hilo Sh64 milioni pamoja na
tani 63 za unga wa sembe pamoja na mahitaji mbalimbali ya kibinadamu
yakiwamo mabati zaidi ya 1,000
NIPASHE
Serikali inakabiliwa na hali ngumu kifedha kiasi cha kushindwa kulipa madeni ya ndani yenye thamani ya Sh. trilioni 1.458.
Miongoni mwa wanaoidai fedha hizo ni watumishi wake, wazabuni, wakandarasi na watalaam washauri.
Madeni hayo yaliwasilishwa serikalini hadi Desemba 31, mwaka jana.
Akizungumza kwenye kikao cha Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Bajeti ambacho kilihudhuriwa na maofisa wa Wizara ya
Fedha wakiongozwa na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Mwigulu Nchemba, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk. Festus Limbu alisema hadi wakati huo ni Sh. bilioni 286.92 tu ndizo zilizokuwa zimelipwa.
Kwa upande wake, Waziri Nchemba alisema
Serikali bado inafanya tathmini ya deni halisi ambalo inadaiwa na itatoa
taarifa ndani ya mwezi huu.
Aidha, Kamati hiyo iliijia juu Serikali
baada ya kubaini kwamba haina nidhamu katika matumizi yake na imetumia
Sh. trilioni 1.426 ambazo hazikuidhinishwa na Bunge.
Alisema matumizi hayo ni kinyume cha
sheria na kwamba jambo ambalo serikali ilipaswa kufanya kabla ya kutumia
fedha hizo ni kurudi bungeni kuomba bajeti ya ziada.
NIPASHE
Serikali inapoteza zaidi ya Sh. bilioni
tano za kodi kwa mwaka kutokana na mafuta yanayodaiwa kwenda nje
kuchakachuliwa na kurudishwa nchini, hivyo kusababisha hasara kubwa.
Kadhalika, serikali kupitia Wizara ya
Nishati na Madini, imetakiwa kuwasimamia wafanyabiashara wa mafuta
kuhakikisha haipati hasara katika mapato yake.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Richard Ndasa, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Alisema mapato ya serikali kupitia
mafuta yanapungua kutokana na Wizara ya Fedha kuwasiliana moja kwa moja
na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) badala ya Wizara ya Nishati na
Madini kinyume cha utaratibu.
“Mafuta yanayoingia nchini asilimia
kubwa kumbukumbu zinaonyesha yanakwenda nje, lakini hayafiki kwa kuwa
yanazunguka na kurudi kutumika ndani bila kulipiwa kodi na kuipotezea
serikali zaidi ya Sh. bilioni tano kwa mwaka…lazima Wizara ya Nishati na
Madini ishirikishwe,” alisema. Ndasa.
Akizungumzia kero ya mara kwa mara ya
kukatika umeme, alisema kamati yake inataka kupata taarifa kutoka kwa
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) pamoja na matatizo ya ukosefu wa
huduma ya mfumo wa Luku yanayoendelea nchini.
Naye Mkurugenzi Mtendaji Tanesco,
Felchesmi Mramba, akizungumzia mfumo wa Luku, alisema matumizi ya huduma
hiyo yameongezeka kutoka watu 300,000 hadi kufikia zaidi ya milioni
moja.
NIPASHE
Wafungwa 14 waliohukumiwa adhabu ya kifo
katika gereza la Isanga, mkoani Dodoma, wamelalamikia ucheleweshwaji wa
nakala za hukumu za kesi zao kwa zaidi ya miaka mitano, hali
inayowakwamisha kukata rufaa.
Kwa mujibu wa taarifa ya wafungwa hao
ofisi ya Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mashariki imekuwa na
ukiritimba katika utoaji wa nakala za hukumu za kesi na hivyo kushindwa
kukata rufaa wakati ni haki yao ya msingi.
Wafungwa hao (majina tunayahifadhi),
walisema Kanda ya Mashariki imekuwa na tatizo katika kushughulikia
suala hilo ukilinganisha na Mahakama Kuu za kanda nyingine ambazo
wafungwa wamekuwa wakipewa nakala za hukumu za kesi kwa ndani ya kipindi
cha mwaka mmoja.
“Sisi wafungwa wa adhabu ya kifo wa
gereza la Isanga Dodoma tunailalamikia kanda ya Mashariki hususan
Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mashariki kwa kutucheweleshea milolongo
na nakala za hukumu za kesi zetu kwa zaidi ya miaka mitano tofauti na
kanda zingine zote ambazo hutoa nakala hizo ndani ya mwaka mmoja tu,”
wameeleza katika taarifa yao.
Waliongeza kuwaa ucheleweshaji huo wa
nakala za hukumu hupelekea kuchelewa kusikiliza rufani zao kwa zaidi ya
miaka kumi tofauti na kanda zingine rufaa husikilizwa ndani ya miaka
miwili tu.
“Baya zaidi maswahibu haya hutukumba
sisi tusio na pesa, mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni, haki
inayocheleweshwa ni haki inayonyimwa, tunamuomba Mwanasheria Mkuu, Jaji
Mkuu na Waziri wa Katiba na Sheria watutatulie kero hiyo kwani siyo wote
tulio gerezani tuna makosa,” wameeleza.
Wafungwa wanaolalamikia suala hilo ni
wale ambao walihukumiwa adhabu ya kifo kati mwaka 1992 ambao idadi yao
ni mmoja, 2003 (mmoja), 2004 (mmoja), 2007 (mmoja), 2009 (wawili), 2010
(watatu), 2011 (watatu) na mwaka 2012 wapo wawili.
NIPASHE
Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania
(BoT), Juma Reli, amejikaanga kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu
za Serikali (PAC), akieleza kuwa benki hiyo haifahamu wala
haijafuatilia taarifa za akaunti 99 zinazodaiwa kumilikiwa kinyemela na
Watanzania kwenye akaunti za siri nchini Uswisi.
Aidha, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
imesema imeanza kuchunguza taarifa zilizotolewa na ripoti ya mtandao wa
Swiss Leaks chini ya Waandishi wa Habari za Uchunguzi wa Kimataifa
(ICIJ) iliyowataja vigogo 99 wenye akaunti za siri nchini Uswisi ili
kubaini majina yao kwa nia ya kuwatoza kodi.
TRA imesema inakadiriwa kuwa takribani
dola za Marekani milioni 328 (Sh. bilioni 574) zinapotea kutokana na
utoroshwaji huo wa fedha.
Katika kikao hicho, majibu ya Naibu
Gavana yalionyesha kuwakera wajumbe wa PAC ambao walimjia juu na kuhoji
sababu za BoT kutofuatilia tuhuma hizo ilhali Serikali ya Uswiss ipo
tayari kutoa ushirikiano.
Aliyeanza kumhoji Reli ni Mbunge wa
Tabora Mjini, Ismail Aden Rage, ambaye alisema Septemba 24, 1998, BoT
ilitoa waraka unaozuia Mtanzania kufungua akaunti nje ya nchi bila
kibali.
Rage pia alihoji kama Watanzania wanafuata utaratibu huo na BoT imeshatoa vibali vingapi.
Akijibu, Reli alisema waraka huo bado
upo lakini akasema watu binafsi hawaufuati kwa kuwa BoT haijawahi
kupokea maombi ya watu binafsi kutaka vibali vya kufungua akaunti nje,
licha ya kwamba wapo wanaomiliki akaunti kwa siri.
Alisema BoT imekuwa ikitoa vibali kwa
kampuni za madini pekee, ambazo hata hivyo, taarifa za akaunti hizo
haziwasilishwi TRA kwa ajili ya kukadiria kodi.
Majibu hayo yaliwakera wabunge na ndipo
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, alihoji kama kwa waraka huo, Watanzania
wanaruhusiwa kufungua akaunti nje.
Swali hilo lilijibiwa na Katibu wa BoT
ambaye pia ni Mwanasheria wa benki hiyo, Yusto Tongola, ambaye alisema
kwa mujibu wa Sheria inayohusu ubadilishaji wa fedha za kigeni ya mwaka
1992, inatoa kibali kwa Mtanzania kufungua akaunti ya fedha za kigeni
nchini, lakini siyo nje ya nchi.
HABARILEO
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti,
imeibana Serikali kuhusu nidhamu ya matumizi ya fedha pamoja na mwenendo
usioridhisha wa utekelezaji wa bajeti yake katika eneo la mapato na
matumizi.
Hatua hiyo ya Kamati ya Bunge imekuja
baada ya kubaini kutokuwepo kwa nidhamu ya matumizi ya fedha za bajeti
ambapo Serikali imekuwa ikitumia fedha nje ya bajeti bila kusubiri
ziidhinishwe na Bunge.
Kamati hiyo ilibaini kuwa kiasi cha Sh
trilioni 1.4 kimeombwa na Serikali nje ya bajeti kwa ajili ya shughuli
maalum kama vile uchaguzi wa Serikali za Mitaa, uandikishaji wananchi
katika daftari la kudumu la wapiga kura na uchaguzi mkuu unaotarajiwa
kufanyika mwaka huu.
“Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC)
imeidhinishiwa kiasi cha Sh bilioni 2.8 kwa mwaka, lakini hadi mwisho wa
nusu mwaka Sh bilioni 16.3 zimeshatolewa kwa shughuli za tume hiyo.
Matumizi haya ni sawa na asilimia 1,148 ya fedha zilizotakiwa kutolewa
hadi nusu ya kwanza na ni sawa na asilimia 574 ya bajeti ya mwaka
mzima,” alisema Mwenyekiti wa kamati hiyo Festus Limbu.
Aliendelea kuhoji kuwa, “Je, ziada hii
haikujulikana tangu awali? Mafungu mengine ya matumizi kama haya ni
pamoja na msajili wa hazina, hali kama hii husababisha mafungu mengine
kutopelekewa fedha kama ilivyoidhinishwa na Bunge.
” Kutokana na mapungufu hayo, kamati
hiyo imeitaka Serikali katika mikakati yake na upangaji wa bajeti
zijazo, kuhakikisha inaweka vipaumbele vinavyotekelezeka kulingana na
mapato yake.
0 comments:
Post a Comment