MKUSANYIKO STORY 10 ZILIZOPEWA HEADLINES KWENYE MAGAZETI YA LEO.. TIZAMA HAPA
MWANANCHI
Mfumuko wa bei kwa mwezi januari umeshuka hadi kufikia asilimia 4.0 kutoka asilimia 4.8 ya Desemba mwaka jana kutokana na kupungua kwa bei za bidhaa mbalimbali ikielezwa kwamba kupungua huko kulikuwa hakujatokea kwa miaka miwili iliyopita.
Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ephraim Kwesigabo alieleza kuwa kushuka huko kumetokana na kupungua kwa kasi ya upandaji bei ya bidhaa na huduma ikilinganishwa na ilivyokuwa Desemba .
Amesema mfumuko wa bei za vyakula na vinywaji umepungua hadi asilimia 4.9 kutoka asilimia 5.7 ya mwezi Desemba.
Ametaja baadhi ya vyakula vilivyochangia kushusha mfumuko huo kuwa ni mahindi yaliyoshuka kwa asilimia mahindi 13.3, unga wa mahindi (6.2), samaki (2), ndizi za kupika (11.3), mihogo (12.0)
Kwa mujibu wa Kwezigabo bidhaa zisizo za chakula nazo zilipungua. Mafuta ya taa yalishuka kwa asilimia 8.4, dizeli (10.2), petroli (6.8) na gesi ya kupikia ilishuka kwa asilimia 2.9. Takwimu hizo mpya zinaonyesha kuwa fahirisi za bei zimeongezeka kutoka 146.0 Januari 2014 , hadi kufikia 152.43 Januari mwaka huu.
MWANANCHI
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amesema chama hicho hakitampitisha mgombea urais asiye na sifa na kuhangaika kumsafisha kwa dodoki ili atakate.
Amesema chama hicho kimeweka mfumo mzuri wa kupata mgombea mwenye sifa, msafi na salama ambaye kazi kubwa itakayokuwapo kwa CCM ni kumwombea kura tu na si kumsafisha.
Alisema CCM ina utaratibu imara ambao utatoa mgombea bora, huku akisisitiza kuwa utawashangaza wengi pale atakapopitishwa mgombea ambaye hakutarajiwa na wengi.
“Mwaka 1995 Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema ‘msinipe mgombea ambaye nikisimama naanza kumsafisha kwanza.’ Tutatafuta mgombea wa kumuombea kura,” Nape alisema jana wakati akizungumza na wahariri wa Magazeti ya Mwananchi na The Citizen alipotembelea ofisi za Mwananchi Communications Limited (MCL), Tabata Relini.
Kauli hiyo ya Nape imekuja siku chake baada ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete kuwataka wenye sifa kujitokeza kuchukua fomu huku akisema: “Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu wa kupata rais wa awamu ya tano, utakuwa wa kihistoria.”
MWANANCHI
Zinaitwa bodaboda, kule Nigeria wanaziita okadas kwa jina jingine ni pikipiki. Hiki ni chombo cha usafiri ambacho katika miaka ya hivi karibuni kimeiteka miji mingi ya Afrika ikiwamo Tanzania.
Licha ya kutumika katika uhalifu, kusababisha vifo kwa kiasi kikubwa, utafiti uliofanywa na gazeti hili katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam ambako kuna matumizi makubwa ya bodaboda ulibaini kuwa usafiri huu unapendwa zaidi na wanawake.
Dereva wa bodaboda katika maeneo ya Tabata Relini, Ayubu Msigala anasema idadi kubwa ya abiria wake ni wanawake. Anasema wanawake wajawazito pia wanatumia usafiri huo kwa kiasi kikubwa.
“Zamani wanawake walikuwa wanaogopa bodaboda, lakini sasa hata wajawazito wanatumia zaidi, hawaogopi kama ilivyokuwa zamani:-Msigalla.
Akizungumzia suala la wanawake kupenda bodaboda, Msigala anasema wanawake waliokuwa wakiziogopa bodaboda sasa ndiyo wanaozipanda kwa wingi huku wanawake wajasiriamali wakiongoza kuzitumia.
Anasema mamalishe, wauza nguo, vocha, hata wafanyakazi wa maofisini wamekuwa wapandaji wakubwa wa bodaboda.
“Hata akina mama wanaokwenda hospitali kupeleka watoto hutumia zaidi usafiri huu ili kuwahi, wakati mwingine naweza kumpakia mama na watoto wake wawili na mzigo,” anasema.
Hata wajawazito wenye kipato cha chini wameelezwa kuzitumia pindi inapowabidi na wengine zimekuwa zikiwapeka kujifungua.
NIPASHE
Tuhuma za kuwapo kwa vigogo wanaoficha fedha katika benki za Uswisi sasa ni dhahiri baada ya ripoti ya mtandao wa Swiss Leaks chini ya Waandishi wa Habari za Uchunguzi wa Kimataifa (ICIJ) kufichua kuwa wapo Watanzania 99 wenye akaunti za siri nchini humo zenye mabilioni ya fedha.
Taarifa ya Swiss Leaks iliyotolewa juzi inaonyesha kuwa Watanzania hao, wakiwamo wanasisa na maofisa wa juu wa serikali, wana akaunti za siri zenye Dola za Marekani milioni 114, ambazo ni sawa na Sh. bilioni 199.6.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania iko nafasi ya 100 kati ya nchi zenye kiasi kikubwa cha dola kwenye akaunti za siri nchini Uswisi.
Msingi wa ripoti hiyo umetokana na aliyekuwa mfanyakazi wa benki ya kimataifa HSBC, Hervé Falciani, kuvujisha siri za akaunti za wateja baada ya kuacha kazi; na mwaka 2008, alivujisha siri za akaunti za siri za baadhi ya watumishi wa umma na wanasiasa wa Ufaransa ambayo mamlaka za kodi nchini humo ilifanya uchunguzi kuthibitisha.
HSBC ni benki kubwa ya biashara duniani ambayo ilianzishwa mwaka 1836. Kwa mujibu wa Swiss Leaks, matokeo ya uchunguzi huo yanatokana na aina tatu za taarifa ndani ya benki kwa vipindi tofauti; Mosi ni taarifa za wateja na uhusiano wao na akaunti za benki nchini Uswisi kwa kipindi cha kuanzia mwaka 1988 hadi 2007.
NIPASHE
Vyama vya vya siasa nchini vinalaumiwa kuteka demokrasia kwa kuwanyima wanawake nafasi za uongozi.
Hayo yalielezwa na wanaharakati wa haki za wanawake wakati wakitoa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu ushiriki wa wanawake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi cha Muhimbili (MUHAS), Dk. Ave Maria Semakafu alisema demokrasia ya Tanzania inawanyima fursa wanawake katika kushika nyazifa mbalimbali za uongozi katika vyama vya siasa huku nafasi nyeti zimeshikiliwa na wanaume.
Alisema wanawake ambao wamebahatika kupata nafasi katika vyama hivyo wamezipata kwa upendeleo, udugu na rushwa ya ngono.“Katika vyama vya siasa wanawake, watu wenye ulemavu na vijana hawajapewa kipaumbele kushika nafasi za uongozi,”alisema.
Alisema katika siasa za Tanzania, vijana wamepewa kipaumbele katika kushiriki vurugu na wanawake wao katika kupiga vigelegele na makofi katika mikutano ya siasa lakini hawapo katika ngazi za maamuzi.
NIPASHE
Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne nchini ya mwaka 2014, yanatarajiwa kutangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Jumapili wiki hii.
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde, alitoa ahadi hiyo kama zawadi kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mpwapwa mkoani Dodoma, kufuatia ajali ya moto iliyotokea Januari 20, mwaka huu na kuteketeza mali zote zilizokuwa kwenye bweni la wasichana 64 wa kidato cha tano na cha sita.
Dk. Msonde alikuwa miongoni mwa viongozi walioongozana na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali zaMitaa (Tamisemi-Elimu), Kassim Majaliwa, kwenye ziara ya kutoa pole katika shule hiyo.
“Zawadi niliyowaandalia ni taarifa kwamba Februari 15, mwaka huu, tutatangaza matokeo ya mitihani iliyofanywa na watahiniwa wa kidato cha nne nchini. Nasema ni zawadi kwa sababu sijaitoa mahali kokote, nyie ndiyo wa kwanza kuipata :-Msonde.
Watahiniwa waliotarajiwa kufanya mtihani huo Novemba, mwaka jana ni 297,488 huku watanihiwa 245,030 wakiwa wa shule na watahiniwa wa kujitegemea walikuwa 52,448. Watahiniwa wa shule walioandikishwa ni wavulana 132,244 (asilimia 53.97) na wasichana 112,786 (asilimia 46.03).
Kwa kawaida, matokeo ya kidato cha nne hutolewa Aprili, lakini mwaka huu yatatoka mapema kutokana na uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu. Walimu ni miongoni mwa watumishi wa serikali ambao hutumiwa kusimamia uchaguzi mkuu.
MTANZANIA
Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, limelazimika kutumia mabomu ya machozi na silaha za moto, kuzima maandamano ya wafugaji wa jamii ya Kimasai kutoka mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, waliokuwa wamejipanga kuvamia Kituo Kikuu cha Polisi Sanya Juu, Wilaya ya Siha mkoani hapa.
Wafugaji hao wanadaiwa walikuwa wakishinikiza kiongozi wao anayeshikiliwa (jina halijafahamika), kuachiwa na Polisi Wilaya ya Siha.
Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kutoka Mjini Moshi waliokuwa na magari manne, walilazimika kutumia nguvu walipokutana na wafugaji hao wakiwa wamefika eneo la mwisho wa lami njia panda ya Karansi na Magadini, Wilaya ya Siha wakielekea kilipo kituo hicho umbali wa kilomita tano.
Habari zilizopatikana jana na baadaye kuthibitishwa kwa njia ya simu na Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Geofrey Kamwela, zilisema makundi ya wafugaji hao yaliingia Wilaya ya Siha kwa nyakati tofauti yakitumia malori, pikipiki aina ya bajaj, bodaboda na magari ya kukodi.
“Kwa sasa niko Siha kwenye operesheni maalum baada ya kuwatawanya wafugaji kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro. Bahati nzuri tumefanikiwa kuzima maandamano hayo yaliyokuwa na lengo la kuvamia Kituo cha Polisi, na hivi sasa tunakusanya taarifa za kiuchunguzi kwa hiyo kesho au baadaye nitatoa taarifa ya kilichotokea:-Kamanda Kamwela.
Kwa mujibu wa Kamanda Kamwela, wafugaji hao ambao idadi yao hadi sasa haijajulikana, licha ya kuingia mkoani hapa wakitokea mikoa hiyo ya jirani kwa ajili ya kuunganisha nguvu na wenzao wa Wilaya ya Siha kutafuta malisho ya mifugo yao, walikuwa wakitumia mbinu mbalimbali kuwakwepa Polisi.
HABARILEO
Bweni la wanafunzi wa shule ya sekondari ya Idodi wilayani Iringa mkoani Iringa, limeteketea kwa moto na kusababisha hasara ya mamilioni ya shilingi, ikiwa ni miaka sita tu tangu bweni hilo liungue na kusababisha hasara kubwa na vifo vya wanafunzi 13.
Agosti 25, 2009 bweni la shule hiyo, liliwaka moto na kusababisha vifo vya wanafunzi wa kike 13, ambao baadhi yao walizikwa shuleni hapo baada ya miili yao kuharibika vibaya.
Katika tukio hilo, wanafunzi wengine 23 walijeruhiwa vibaya, baada ya bweni hilo kushika moto uliosababishwa na mshumaa uliowashwa na aliyekuwa mwanafunzi wa shule hiyo, Naomi Mnyali ambaye alisahau kuuzima baada ya kumaliza kusoma.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka eneo la tukio, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto mkoani Iringa, Inspekta Kennedy Komba alisema kuwa bweni hilo limeteketea lote na kuunguza baadhi ya mali, zikiwemo za wanafunzi zilizokuwemo katika bweni hilo.
Alisema taarifa za awali zinaonesha chanzo cha moto huo, kilitokana na hitilafu ya umeme na kwamba hakuna mwanafunzi yeyote aliyejeruhiwa katika tukio hilo. Komba alisema kuwa baada ya jeshi la zimamoto kupata taarifa ya tukio hilo, lililotokea kati ya saa 3 na 4 jana asubuhi wakati wanafunzi wa shule hiyo wakiwa darasani, iliwachukua dakika 45 kufika katika eneo la tukio.
Alisema baada ya kufika katika eneo la tukio kutoka Iringa mjini ambako ni umbali wa kilometa 40, kazi ya kuuzima moto huo haikuwa kubwa, kwani wananchi waliofika kutoa msaada, walifanikiwa kuzima moto huo kwa kiasi kikubwa. Aliwapongeza wananchi kwa moyo wa ushujaa wa kujitolea na kuwataka kutoa taarifa mapema pindi majanga ya moto, yanapojitokeza katika maeneo yanayowazunguka.
“Endapo tungepata taarifa mapema ninaamini tungeweza kuokoa vitu vingi zaidi,” alisema Kamanda huyo na kuwataka wananchi wasitegemee mtendaji au kiongozi apige simu kwa kikosi cha kuzima moto kwani kila mtu ana fursa ya kupiga simu 111 katika kitengo cha mawasiliano cha jeshi hilo”.
MTANZANIA
Upande wa Mashikata kesi inayomkabili Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda umewasilisha ushahidi muhimu wa mkanda wa video unaodaiwa kuonesha uhalisia wa tukio zima la kesi yake inayomkabili ya kutoa maneno ya uchochezi.
Mkanda huo wa video uliletwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, Mary Moyo na kuoneshwa na shahidi wa tano wa kesi hiyo ambaye ni askari kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi kitengo maalumu cha uchunguzi wa picha, Aristides alieleza vigezo alivyovitumia kuitambua uhalisia wa video hiyo iliyochukuliwa Agosti 10 mwaka 2013.
Shahidi huyo akiongozwa na Wakili wa Serikali, Benard Kongola alieleza mahakamani hapo kuwa video aliichunguza na kugundua kuwa ilichukuliwa katika eneo la tukio kupitia kamera ndogo aina ya JVC na kwamba baada ya kuichunguza aliandika hati na taarifa iliyoeleza vigezo alivyovitumia katika uchunguzi huo na yale aliyoyaona na kuyasikia katika video hiyo ambayo aliitoa mahakamani kama kielelezo.
Pamoja na ushahidi wake, lakini pia aliionesha video hiyo mahakamani hapo ambapo ilionesha tukio zima pamoja na maneno aliyoyatoa Shehe Ponda ambayo yanadaiwa kuwa yalikuwa ya uchochezi na yaliyoumiza imani ya dini nyingine.
Shahidi huyo pia alitoa kamera, DVD, hati na taarifa ya uchunguzi wa video hiyo kama kielelezo na kupokewa na mahakama hiyo.
MWANANCHI
Baada ya kumalizika mkutano wa 18 wa Bunge Jumamosi iliyopita, wabunge wengi wamekimbilia kwenye majimbo yao hatua inayohusishwa na homa ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Tofauti na kawaida ya wabunge wengi ambao baada ya vikao vya Bunge hukimbilia Dar es Salaam, safari hii wengi wameelekea majimboni kuweka mikakati ya kuhakikisha wanarudi bungeni katika uchaguzi huo.
Baadhi ya wabunge waliohojiwa jana wameelezwa kuwa wako katika mikakati mbalimbali ya kupambana na wapinzani wao watakaojitokeza kuwania nafasi hiyo.
Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Stephen Ngonyani jana alikuwa kwenye mazishi ya rafiki yake na taarifa zinasema kwamba baada ya mazishi hayo ataendelea na shughuli zake za jimbo.
Mbunge wa Tanga Mjini (CCM), Omar Nundu, Mbunge wa Lushoto (CCM), Henry Shekifu, Mbunge wa Mkinga (CCM), Dastan Kitandula, Mbunge wa Muheza (CCM), Herbert Mtangi wapo majimboni mwao wakiendelea na shughuli zao.
Imeelezwa pia kwamba wabunge Yusuph Nassir (Korogwe Mjini – CCM), Saleh Pamba (Pangani – CCM) wako Dar es Salaam wakijipanga kurudi majimboni mwao kufanya mikutano na shughuli zao za kisiasa.
0 comments:
Post a Comment