Jinsi ya kumfurahisha mwanamke wako, Atamani kuwa na wewe karibu kila Mara, Cheki hapa.
KUMFURAHISHA mwanamke ni jambo ambalo wanaume walio wengi wangependa
kulifikia na kila mmoja anayejiingiza katika uhusiano wa kimapenzi na mwanamke hujitahidi kutaka kumfurahisha. Hata hivyo, si wengi wanaofanikiwa kufikia lengo hili. Tena zaidi ya hapo, amini usiamini, hupaswi kwa sababu yoyote ile kujitahidi kumwonesha mwanamke kuwa unamfaa, kwa kujitahidi kumfurahisha.
Lakini japo mwanamke hatarajii kuwa utamtendea miujiza katika mapenzi, mathalani kumpeleka kutalii mwezini, kuna mambo mbalimbali ambayo wanawake hutarajia kufanyiwa na wanaume. Hata hivyo, kwa afya yake, mwanaume anapaswa kuwa makini anapopanga kumfurahisha mpenzi wake. Tangu siku ya kwanza unapokwenda nyumbani kwa mwanamke kwa ajili ya kumtamkia suala la mapenzi, au kuendeleza uhusiano ulioanza wiki moja iliyopita, kwa vyovyote vile utakuwa na heshima ya kiasi fulani kwake. Angalau kwa asili wanaume wengi wanalifahamu hilo. Lakini pia, mwanamume hupaswa kumtendea mema mwanamke. Baadaye kadri siku zitakavyokwenda, tena kama mmebahatika hata kuoana na sasa mmeishi miaka kadhaa, unaweza kushangaa ni kwa jinsi gani mwanamke anavyoweza kukumbuka mambo madogo uliyomfanyia.
Bila kujali kuwa baadaye tabia yako kwake itakuwa vipi, unapaswa kuhakikisha kuwa mwanzo wenu unakuwa wa kishindo. Lakini wakati huo huo, hakikisha kuwa unaonesha makucha yako wakati huo wa mwanzo, mathalani kama kuna jambo la kukukasirisha, kasirika na wala usibane hasira zako kifuani, kwani ukiachilia mbali suala la mustakabali wa mapenzi, kubana hasira kutakuumiza wewe mwenyewe. Pia katika siku za kwanza za kukutana na mpenzi wako, ni wazi kuwa utajitahidi kumshirikisha katika mazungumzo ya kusisimua na kumwonesha kuwa una hisia za furaha.
Ni furaha iliyoje wakati mwanamke anapojihisi kuwa ataishi maisha ya furaha na mwanaume aliyempenda? Baada ya kudhihirisha jinsi ulivyo mwema na mwenye furaha mbele yake, yamkini pia utapaswa kujitahidi kuwahakikishia hilo wazazi wake pia. Ni mtu gani ambaye hapendi wazazi wa mpenzi wake waridhie uhusiano wake na binti yao? Hayupo. Hata wanawake hupenda wazazi wa wanaume kutambua na kubariki uhusiano wao. Mara nyingi kama azma ya msichana na mvulana ni kuoana, kila upande utataka wazazi wa upande mwingine wafahamu kuchanua kwa penzi lao na kuridhia hatua hiyo.
Wazazi wanapofahamu hukutua mzigo mabegani mwako na tangu wakati huo utajisikia vema kwani hujioni tena kama mwizi. Hapa hakuna kazi kubwa. Isipokuwa unapaswa kuzingatia mambo mawili; nayo ni kumfurahisha baba wa mpenzi/mchumba wako kwa werevu wako na kuiteka roho ya mama kwa uchangamfu wako. Katika kuhakikisha haya yanafanyika, utalazimika kujadiliana na mzee masuala mbalimbali kuhusiana na siasa pamoja na mambo ya ufahamu wa jumla, huku ukionesha kuwa unafahamu mambo na baadaye kusifu mapishi ya mama.
Haya mambo yote yanapaswa kufanyika huku pia ukihakikisha kuwa unapokwenda kwa wazazi unavaa vizuri, na unajiamini katika matendo na mazungumzo yako, ili usije kuonekana kama mwizi. Wazazi wangependa kuona mtoto wao akiishi na mtu mwenye heshima, anayejijali na mwenye
ufahamu. Kama yote haya umeyafanya lakini msichana unayemfukuzia bado hajakuchangamkia, unapaswa kuwa na wasiwasi kama kweli anakupenda. Kwa hiyo mbinu nyingine unazoweza kuwa umezihifadhi zinaweza zisikusaidie, kama kufikia hapo mwanamke hajashtuka. Wakati mwingine watu hupitiliza kipimo wanapokuwa mbioni kuwanasa wanawake waliowapenda. Unapozidi kipimo utabainika lakini mbaya zaidi ni kwamba unaweza kuchoreka tu na bado mambo yako yasiwe mazuri baadaye. Kuna mambo kadhaa ambayo ukijikuta unayafanya, fahamu kuwa umechemsha, yaani umevuka mpaka katika suala zima la kutaka kumfurahisha mwanamke ili akupende. Tena kama una mambo haya, fahamu kuwa umekuwa na mapenzi yasiyo na macho, pengine kutokana na tamaa kubwa uliyo nayo kwa mwanamke huyo. Ifuatayo ni mifano ya matendo ambayo hupaswi kuyafanya kwa ajili ya kumfurahisha mwanamke:-
1. KUVUKA MPAKA KATIKA KUONESHA MAHABA Katika kujaribu kumfurahisha mpenzi unaweza kufanya jambo, lakini jambo hilo likavuka mpaka, au likapuuzwa. Mathalani unaweza kutaka kumteka kwa kuimba nyimbo za mapenzi, lakini kumbe yeye mawazoni mwake akakuona kuwa hufai kuimba na hata akawa anaisikia sauti yako kama kelele. Wakati mwingine unaweza kumpa sifa kubwa zisizowezekana au zilizo nje ya ufahamu wa mwanadamu, mathalani unapoulinganisha urembo wake sawa na wa malaika. Unaweza kuonekana mjinga au mtu asiyekuwa makini kwa kutamka maneno kama hayo. Wasichana wengi hawapendi kuambatana na wavulana wanaojifaragua katika mambo mbalimbali, kwani wengi wao huamini kuwa mwanaume ni mwongo tu. Unapaswa kufanya jambo ambalo una hakika utathibitika kuwa unalifanya kwa madhumuni ya kimapenzi na si vinginevyo.
2. KUKUBALI KUPELEKESHWA NA MWANAMKE Usifanye jambo lolote linaloweza kukufanya udhalilike utu wako kwa mwanamke . Njia mojawapo ya kufanya jambo hili ni kumpitia mwanamke kila siku kwa ajili ya kumpeleka kazini, kiasi kwamba ukawa kama dereva wake – hususan kama hajakubali kuwa mpenzi wako. Kumchukua mwanamke na kumpeleka kwa gari lako kila anakotaka kwenda hakuna uhusiano wowote na mapenzi. Wala kufanya hivyo hakuwezi kudhaniwa kuwa na maana sawa na ‘nakupenda’, bali badala yake kitu unachojaribu kubainisha ni kwamba unapelekeshwa na mwanamke. Kosa jingine wawezalo kulifanya wanaume katika kipindi hiki ni kujaribu kuyapa nafasi kila matakwa ya mwanamke. Hakikisha kuwa huyatoi kafara maslahi yako kwa ajili ya maslahi ya mwanamke ili umfurahishe. Kama unafahamu kuwa mwanamke huyu hawezi kukubali kuangalia mchezo wa mieleka kwenye televisheni na wewe, hakuna haja ya kwenda naye kila unapokwenda kuangalia televisheni. Umuhimu wa kuepuka kutekwa kihobi na mwanamke ni kujihakikishia kuwa hakutawali. Ili uweze kujihakikishia suala hili, mwoneshe mwanamke kuwa unamtaka tu kimapenzi kama unavyoweza kumtaka mwanamke mwingine. Pia kwa kufanya hivyo utabaini na kuiridhisha roho yako kuwa lengo pekee la wewe kuwapo duniani si kumfurahisha yeye, kwani unayo mambo mengine muhimu ya kufanya. Kwa kuendelea kuwa na akili yako (wengine akili zao hutekwa na wanawake), unajihakikishia nafasi ya kupendwa kwa uhakika zaidi na mwanamke huyo au mwingine. Kumbuka unapojijengea mazingira ya kupendwa kuna raha zaidi kuliko ukipenda wewe, maana katika kupenda kuna kuteswa pia. Usikubali kujitishwa mzigo mzito wa kumfurahisha mwanamke.
3. KUJARIBU KUMVUTA KWA PESA Wanaume wengi hudhani njia ya kuingilia kwenye moyo wa mwanamke kwa ajili ya kuuteka ni kutumia fedha. Hata hivyo, wasichana wengi hawawapendi wanaume kutokana na ukubwa wa mifuko yao – na hata wale wachache wanaoingia ‘line’ kwa sababu ya pesa wanapaswa kuogopwa kama ukoma, maana kwa hakika hawana mapenzi ya kweli. Hakikisha kuwa hujisumbui kumpa mwanamke huduma ya VIP, kwani siku uwezo wako wa kutoa huduma hizo ukiisha naye ataondoka. Lakini kama una uwezo wa kutosha wa kumpa hata dunia nzima basi mpe, lakini ujue kuwa akikupenda kwa njia hii atakuwa ameipenda zaidi fedha yako. Hata hivyo, kwa wale akina yakhe wasio na rasilmali kubwa na kazini kwao mishahara yao ni ya KCC, usilazimike kuchagua migahawa ya kifahari kwa ajili ya chakula cha mchana na mpenzi wako, bali mwache akuthamini kwa kile kidogo unachofanikiwa kumfanyia.
4. KUMWOMBA RUHUSA KILA MARA Ni wazi kuwa baadhi ya wanaume hutaka kuwaonesha wanawake kuwa ni waadilifu na wenye unyenyekevu wa kutosha, kwa hiyo unamwomba ruhusa ya kwenda kukutana na marafiki zako kijiweni badala ya kumuaga tu na kujiondokea. Hii ni mbaya sana, na hasa zaidi kama mwanamke mwenyewe hujakubaliana naye lolote la maana na huishi naye. Jiulize, kwa nini umpe mwanamke uliyekutana naye juzi tu mamlaka juu ya utashi wako? Kumbuka ninyi si mapacha walioungana, kwamba mnalazimika kuwa pamoja kila mara, wala hamjafunga ndoa, sasa kwa nini usiwe huru kufanya mambo unayoyataka kwa wakati unaoutaka? Je, wewe humhitaji mwanamke anayekuamini na kukupa uhuru wa kufanya mambo kwa wakati wako, bila kulazimika kuomba ruhusa? Ni wazi kuwa unataka uhuru, yeye naye anapaswa kufahamu. Usikubali kuukosa uhuru huo na ikibidi mkose yeye.
5. KUKUBALI LAWAMA KWA KILA JAMBO Inawezekana mara kwa mara umejikuta ukimwambia mwanamke ‘samahani’, wakati mwingine ukiwa hata huna makosa. Je, unataka kujiwajibisha kwa kila jambo litakaloonekana baya machoni pa mwanamke kwa lengo la kumfurahisha? Kama jibu ni ‘ndiyo’, yaani kama unaomba radhi ili kuhakikisha kuwa kila wakati mwanamke wako ana furaha, unakosea na huo si uanaume. Lakini mbaya zaidi, usijidhanie kuwa utapendwa na kuheshimiwa kwa hilo, sana sana utadharauliwa. Unapomfanya mpenzi wako kujiona kama mtakatifu fulani ambaye hawezi kukosa, unakuwa unakosea. Ni hatari iwapo hali hii utaondoka nayo katika uchumba na kwenda nayo katika maisha ya ndoa, maana sasa utakuwa sawa na mtumwa kwa mkeo. Kama utabaini mara kwa mara kuwa mpenzi wako amekosa, usikubali kuomba msamaha kwa kosa lake, bali mweleze kuwa ni kosa lake. Kama kweli ndiye aliyepangwa kuwa mkeo (sijui mpangaji nani), basi ni dhahiri kuwa atakuelewa na yeye ndiye atakayeomba radhi kwa makosa yake na zaidi ya hayo hatataka kukutia hatiani kila mara
.
UKWELI, UWAZI, KUJISIMAMIA Jambo muhimu unalopaswa kuzingatia katika uhusiano wako wa kimapenzi na mwanamke, hasa katika hatua za awali za uhusiano huo, ni kuhakikisha kuwa unakuwa mkweli na mwazi kisha kujisimamia. Ukiyaweza haya mambo matatu bila msaada wowote, utafahamu kama kweli anakupenda
0 comments:
Post a Comment