Rais Kikwete Aombwa Kutoupitisha Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandaoni, 2015 ....Ombi Hili Limetolewa Na Chama cha Bloggers Tanzania (TBN). cheki hapa.

SOCIALIZE IT ⇨


Mtandao wa waandishi kupitia mitandao nchini, Tanzania Bloggers Network (TBN) tunamuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kutumia mamlaka yake vyema kwa kutokupitisha muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao, 2015 unaokandamiza uhuru wa mawasiliano mitandaoni.

Muswada wa sheria ya makosa ya Mtandaoni unaainisha makosa yanayohusiana na matumizi ya mfumo wa kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, na kuweka utaratibu wa upelelezi, ukusanyaji na matumizi ya ushahidi wa kieletroniki na masuala mengine yanayohusiana na hayo.

Muswada Wa Sheria Ya Makosa Ya Mtandaoni,2015
Umoja huu (TBN) ulishtushwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukubali kupitisha Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao 2015 kwa hati ya dharura kitendo ambacho hakikutarajiwa kutokana na kuwa mitandao bado ni kitu kipya nchini hivyo tulihitaji maridhiano na wadau na elimu kati ya raia na Serikali ili wengi watambue yapi ni makosa kwa kutumia mitandao na yapi yanakubalika

Kimsingi TBN haipingi Tanzania kuwa na Sheria ya Makosa ya Mtandao bali inaiomba Serikali kuwashirikisha wananchi na hasa wadau wa habari na wanamitandao ya jamii ili kuridhiana kwa vipengele ambavyo vinaonekana kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari. Na hatimaye kutoka na sheria isiyo na viashiria kandamizi juu ya uhuru wa kupata na pokea habari.

Hali kadhalika tulishuhudia watetezi wa haki za binadamu pamoja na wawakilishi wa watumiaji wa Mtandao wa intaneti nchini wakitoa sababu zenye uzito za kwanini sheria hii isipite kwa hati ya dharura na kuhoji kwanini sheria hii ipite kwa dharura bila ya kupata majibu.

Muswada huu ambao kati ya makosa mengi uliyonayo kubwa moja wapo ni majukumu makubwa aliyopewa Mkuu wa Kituo chochote cha Polisi kuwa na uwezo wa kupekuwa na kuchukua vielelezo/data pale anaposhuku kuna suala la uhalifu unaohusu mtandao. Swali ni kuwa kwanini polisi apewe mamlaka ya kumsulubisha mtuhumiwa katika hatua ya mwanzo bila uthibitisho sahihi?

Mbali na hapo, sisi kama waandishi ulimwenguni kote tunatakiwa kufuatilia maadili ya kazi zetu. Maadili ya mwandishi yeyote yule ni kutunza usiri wa chanzo cha habari yake pale inapotakiwa lakini katika sheria hii sisi kama bloggers, sheria hii inakiuka hili kwa kutulazimisha kutaja vyanzo vya habari.

Kupitia sheria hii, bloga yeyote yupo hatarini kutokana na kwamba sheria inaainisha ni kosa la jinai kutoa ujumbe unaoweza kumuudhi mtu kihisia.

Aidha, tunamuomba Mheshimiwa Rais pia asipitishe Muswada wa Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2013.

Muswada huu unavinyima uhuru vyombo vya habari vinavyotangaza takwimu mbalimbali. Kama ilivyo Ibara ya 7(4) ‘‘Chombo chochote cha habari ambacho kinachapisha taarifa za kitakwimu za uongo au upotoshaji, au kinatangaza kipindi chochote kinachohusu shughuli za ukusanywaji wa taarifa ambayo imefanywa au inafanywa na Ofisi, na hatimaye kusababisha wananchi wasishiriki kwenye shughuli hiyo ya ukusanywaji wa taarifa au wasishirikiane na maafisa wa Ofisi, kinatenda kosa.’’

Hii inamaanisha kuwa hata blog zetu ziko hatarini kuelekea katika kulazimika kufanya kazi za kuisifia serikali na kutangaza takwimu zilizopitiwa na serikali tu, jambo ambalo litaharibu ukuaji wa uhuru wa habari nchini.

Tunamkumbusha mwananchi wa kawaida anayetumia mtandao wa intaneti kuwa hayuko salama kwani sheria hii inamlazimisha mtoa huduma wa mtandao kutoa taarifa za wateja wake jambo ambalo linahatarisha uhuru wa kutoa na kupokea habari.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika

IMETOLEWA NA;
Chama cha Bloggers Tanzania (Tanzania Bloggers Network-TBN)
04/03/2015.
http://www.tbn.or.tz/

0 comments:

Post a Comment